Napenda kuwasalimu watu wote na pia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa pumzi anayoendelea kutupa ingawa kuna wenzetu waliotangulia mbele za haki kwa sababu tofauti tofauti lakini hiyo yote ni kazi yake haina makosa.
Chunusi ni aina ya vipele vinavyotokea kwenye uso wa binadamu hasa wakati wa kubalehe na Msasa ni aina ya kifaa kinachotumiwa na mafundi ujenzi katika kutolea vitu vinavyofanya sakafu isiwe katika msawazo.
Vitu hivi ni viwili tofauti kabisa na wala haviendani na ndio maana nahisi utakuwa unajiuliza kwa nini nimevihusisha sehemu moja lakini ukweli ni kwamba kuna dawa za chunusi ambapo ukiwaona wataalamu wa magonjwa ya ngozi watakusaidia kuweza kupata tiba sahihi hivyo kwa makala hii nimefananisha chunusi na vitu vinavyotokea juu ya sakafu au ukuta kwani nazo zinafanya sura isiwe katika hali yake ya kawaida. Ukitaka kuondoa chunusi huwezi kutumia Msasa lakini utatumia dawa kwani Msasa utamuumiza mtu na kupata madhara makubwa.
Baadhi ya wananchi wa Tanzania wanaonekana kutaka kutoa chunusi kwa Msasa ili kuwaumiza wananchi kwa ujumla kwani kitendo cha kuzomea na kutomtaka mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuongea na kutoa hoja zake si kitendo cha kiungwana hata kidogo tena ukizingatia kinafanywa na wasomi wanaotegemewa na jamii hivyo kupinga usemi wa Wasomi wanabishana kwa hoja tena kwa kupokezana na si kupayuka kama kwenye klabu za pombe ya kienyeji.
Kulikuwa na makongamano baadhi yaliyoitishwa na UDASA pale Chuo kikuu cha Dar es salaam katika kujadili suala la kupata katiba mpya lakini katika kongamano zote kuna watu waliozomewa kwa kuongea hoja zinazoitetea serikali iliyopo madarakani na jana tena Mbunge wa CCM alizomewa pia kutokea kwa vurugu pale Dodoma ni viashiria tosha kuwa watu hatutaki kujenga hoja bali kujenga uhasama ndani ya mioyo ya watu watulivu.
Kwa jinsi nionavyo wananchi washajijengea kuwa Mtoto wa Nyoka ni Nyoka hivyo kuamini kila mwana CCM akisimama yatakuwa yaleyale tu lakini sivyo kwani nakumbuka Katibu wa CHADEMA, Dr Wilbrod Slaa alivyompigia debe Mh. Harrison Mwakyembe kipindi cha uchaguzi bila kuangalia chama hiyo ilitudhihirishia kuwa kuna watu wachapa kazi bila kuangalia wapo katika chama gani sasa nashangaa sisi tunavyokataa kuwasikiliza wana CCM.
Kuendelea kutumia njia tunayoendelea kuiamini ni kupotoka na kukosa mwelekeo wa kufikia vitu tunavyovihiyaji na kugeuka kelele za chura ambazo hazitamnyima Tembo kunywa maji bali tukikaa na kujua njia sahihi ya kutumia kwa kutumia usomi wetu huu huu naamini tutafanikiwa bila kutoa jasho jingi kama tunaloangaika nalo sasa hivi bila kujua hatima yetu ya mbeleni kwani wengi wetu tunapelekwa pelekwa tu bila kujua tuyafanyayo.
Hivyo njia tunayoitumia katika kudai haki ni sawa na Msasa ambao si jibu au dawa sahihi ya Chunusi ambazo ni kama matatizo tunayoyapigia kelele kila kukicha hivyo umoja tuliokuwa nao ni mzuri lakini kama hauna malengo imara na njia madhubuti hautasaidia kitu.
Imeandikwa na N.Mugittu
NIJUE KWA UFUPI
Jina langu ni Neligwa Boaz Mugittu, mtoto wa tatu katika familia yenye watoto wanne nikiwa mtoto wa kiume pekee. Baba yangu anaitwa BOAZ MUGITTU ambaye kwa sasa ni marehemu tangu atutoke 26/6/1998 na kubaki na mzazi mmoja tu ambaye ni Mama yangu kipenzi aitwaye ESTHER PHILIP NAPUNIGWA ambao wote ni WANYIRAMBA kwa kabila na Wakristo katika dhehebu la LUTHERAN. Dada yangu wa kwanza anaitwa CHRISTOWELLU ambaye naye ana familia yake anayoishi nayo huko BUNJU, dadangu wa pili anajulikana kama WANONDA aliyetangulia mbele ya haki 21/4/2002 na baada ya wao ndio akatokea kidume chao NELIGWA 8/3/1990 ikiwa ni siku ya Wanawake duniani na wa mwisho ni mdogo wangu aitwaye TYATAWELLU. Nyumbani kwetu ni Ukonga Mombasa na ki elimu ni mwanafunzi katika chuo cha MLIMANI nikichukua Stashahada ya Uandishi wa habari. Elimu ya msingi nilimalizia LUPALAMA 'A' iliyopo Iringa au TOSAMAGANGA HOME BOYS, kidato cha nne nimemalizia KINDOROKO iliyopo MOSHI na kidato cha sita ni TUNDURU iliyopo RUVUMA. Shule nyinginezo nilizosoma ni KURASINI iliyopo Temeke jijini Dar, UKONGA iliyopo Ilala jijini Dar na MWANDU ya Iguguno mkoani Singida zote kwa elimu ya msingi na sekondari ni KALENGA iliyopo Iringa na Juhudi iliyopo Dar. Hiyo ni historia yangu kwa ufupi mengine tutazidi kufahamishana. Nawapenda wote